EDSON MWASABWITE: NI KWA NEEMA TU

Monday, March 17, 2014

ISEMAVYO MITANDAO: EDSON MWASABWITE MWIMBAJI ALIYETOKA MBALI

Habari inatoka: FREE MEDIA/TANZANIA DAIMA

  • Asema alivyo leo ni kwa neema tu ya Mungu
  • Wadau Tamasha la Krismasi Moro wamhitaji 
  • Asema yu tayari kuimba kama atajumuishwa
“HAPA nilipo mimii ni kwa neema ya Mungu, vile nilivyo mimi ni kwa neema ya Mungu, nimetoka mbali-toka mbali toka mbalii nimetoka mbaliii…… Ni kwa neema tu na rehemaa, ni kwa neema tu na rehemaa.”
Hayo ni baadhi ya maneno katika
wimbo wa ‘Ni kwa Neema na Rehema’ uliomtambulisha vema kijana Edson Mwasabwite, ambaye kwa sasa ana albamu  moja yenye jumla ya nyimbo nane ikibebwa na wimbo huo, huku akiwa mbioni kukamilisha albamu
yake ya pili.
Albamu hiyo yenye nyimbo za kutia faraja, kusifu na kuabudu ilianza kupendwa mkoani Iringa na Mbeya ambako watu wengi hupenda kusikiliza wimbo wa ‘Ni kwa Neema na Rehema’.
Akiwa ametambulishwa vema na albamu hiyo, Mwasabwite anasema ana kila sababu ya kumshukuru Mungu alipofikia kwa kuwa amekutana na changamoto nyingi sana wakati anaanza kuimba
kama mwimbaji binafsi.
Edson aliachwa yatima kwa kuondokewa na wazazi wake ambapo wimbo wa ‘Ni kwa Neema na Rehema,’ amesema amejaribu kuelezea jinsi neema na rehema ya Mungu ilivyomtetea na kumfikisha  alipo, maana asingekuwa Mungu labda ingebaki historia tu kutokana na maisha magumu aliyopitia. Amesema yeye ni kijana aliyeokoka, anampenda Mungu, anaabudu katika Kanisa la Kilutheri Kijitonyama, jijini Dar es Salaam.
Kilio chake Edson kwa waimbaji wenzake ni kuwasihi kuwa barua inayosomwa vema na wanaowahubiria
ili maneno na matendo yawe sawa na kubariki pamoja na kuwavuta watu
kwa Yesu zaidi kuimba kwao isiwe hapa duniani pekee bali siku moja wakajiunge na jeshi kubwa la malaika mbinguni.
Edson anawasihi waimbaji wasiwe kama vibao kuishia kuonesha njia wakati vyenyewe haviendi huko kunakotakiwa.
Anasema kuwa hafungwi kuabudu katika kanisa lolote na ikiwa atapokea maono  ya kuhama, basi atafanya hivyo.
Anasema wimbo wake wa ‘Ni kwa Neema na Rehema’, aliimba kwa sababu hakutarajia kama angefika alipo, kwani ni kwa neema tu, kwakuwa aliishi maisha magumu baada ya kuachwa yatima.
“Hii ni historia ya maisha yangu. Wokovu wenyewe ni kwa neema, nikiangalia vijana wengine mimi niko salama zaidi,” anasema.

Mafanikio
“Mafanikio yapo, japo kwa mtu mwingine yanaweza kuonekana kama sifuri, ila mafanikio inategemea na huyo mtu yuko katika nafasi au ngazi gani. Ingawa ndiyo nimeanza, naona mafanikio, namshukuru Mungu,” anasema.

Changamoto
Edson anasema changamoto katika uimbaji zipo, hasa kwa chipukizi, kwani  mtu anapoanza kuimba unakuta hana fedha, mara nyingine inakuwa ni kikwazo ili kuweza kuweka uimbaji katika viwango vya juu.
Anasema changamoto nyingine ni watu wengine kushauri vibaya kwa makusudi ili uanguke.
“Hakuna ushirikiano kwa wale walio wazoefu katika muziki wa Injili, hii imesababisha hata hasara, kwa kuwa unakosa  mwongozo kutoka kwa wazoefu.
“Lakini pia kuna changamoto ya utaalamu, wasikilizaji na jamii kwa ujumla hawajaupa nafasi sana muziki wa injili. Watu wengi wanauchukulia kama burudani tu, suala la kuelimisha na kusisimua.
“Ila tunashuru Mungu kwamba watu wanatuunga mkono. Ndiyo maana utakuta nyimbo zinazohit ni zile za kuburudisha zaidi. Kwa Tanzania Mungu ameupa muziki wa Injili Neema,” anasema.
Anaongeza kuwa, kwa sasa anaishi Dar es Salaam. Kuhusu suala la kuoa anamuomba Mungu ampe mke mwema, kwani ni heri ukosee kujenga nyumba au kurekodi wimbo utaurudia lakini si kuoa.
Ushauri
Ujumbe wangu kwa waimbaji wenzangu wa nyimbo za Injili, wajue kama unahubiri, uwe mfano na wakili, tusiwe kama vibao, lakini tusiende huko. Yesu alisema itamfaa nini mtu apate vya dunia na kuikosa mbingu.
“Wito wangu kwa watu wote ni wawe tayari kuelimishwa pia na nyimbo za Injili na si kuburudika tu, wajue tunaishi kwa neema tu, wajue Mungu ndiye ametupa vyote tulivyo navyo, ambao hawajaokoka wampokee Yesu Kristo.
Vyote tulivyo navyo bila Kristo ni bure, wajiulize wataishi wapi baada ya maisha haya.
“Tuwe barua, mtu akituona ajue kweli huyu anamwimbia Mungu aliye hai. Tujiandae kuimba mbinguni, si kupata sifa hapa duniani na kwa waimbaji chipukizi, kwa wanaoanza wasikate tamaa, kwani hakuna aliyezaliwa akiwa na jina, wala vitu, wawe wavumilivu na waaminifu mbele ya Mungu ili wafanikiwe,” anasema.

Historia
Edson alizaliwa Meta, Mkoa wa Mbeya, Aprili  24, 1983 na kupata elimu ya msingi Mtaba.
Anasema kuwa kipaji chake cha uimbaji kilitambuliwa akiwa Shule ya Jumapili ‘Sunday School’ Rungwe, mkoani Mbeya.
Anasema kuwa katika familia yao wamezaliwa watoto watatu kwa upande wa mama yake.
Anaeleza kuwa yeye ni mtoto wa nje ya ndoa na alilelewa na mama yake, ambapo hakumfahamu baba yake hadi alipofika darasa la nne.
“Nimeishi maisha magumu sana yenye changamoto za kila aina, yaani unaishi na mama ambaye ni mkulima, maskini na kama unavyojua maisha ya  kijijini wakati mwingine hakuna kula, kuni zimelowa au kukosa hela ya chakula,” anasema.
Anasema kuwa baada ya kumfahamu baba yake alikaa naye kwa miaka mitatu na akafariki dunia mwaka 1999 na ndipo matumaini ya kusoma yakapotea. Anaeleza kuwa miaka michache baadaye mama yake alianza kuugua.
“Nilimuuguza mama yangu huku nikilea familia, aliugua kwa muda wa mwaka mmoja na nusu na alifariki dunia mwaka 2005, yaani hapo ndoto zote zilikufa, ila namshukuru Mungu maana mimi niliokoka mapema, ilinisaidia kutokujiunga katika makundi ya kihalifu, maana hofu ya Mungu ilikuwa ndani yangu,” anasema.

Mbio za umaarufu
Anasema kuwa mbio zake za uimbaji zilianza rasmi mwaka 2007 na kuanza kutafuta michango, lakini hakupata.
“Kuna watu siwezi kuwasahau, walinisaidia sana katika harakati zangu za uimbaji, yaani mtu kama Angonile, Sifa Mwankili na Mama Nisa, hawa walikuwa wakinipatia fedha na hata kunikopesha, ila sikufanikiwa na nikarudi kijijini,” anasema.
Anaeleza kuwa baada ya mwaka huo kutofanikiwa alirejea tena Dar es Salaam  2010 akiwa hana mfadhili, anasema kuwa maisha yalikuwa magumu sana japo alifanikiwa kurekodi albamu hiyo.
“Baada ya kurekodi, nilirudi nayo kijijini na ndipo niliugua TB, nikatibiwa na kupona, lakini maisha yakawa ya taabu sana,  nikawa sina hela, madeni mengi, kazi haipo sokoni, ninayo ndani,” anasema.
Anasema hawezi kumsahau Ephraim Mwansasu, kwani ndiye aliyemsaidia kumpeleka kwa wasambazaji na albamu hiyo ambayo inapendwa na wengi.

Usiyoyajua
-Muimbaji huyo hajaoa, hana mtoto.
-Albamu yake ya ‘Ni Kwa Neema na Rehema’ aliirekodi mwaka  2010.
-Alikuwa akifanya biashara ya kahawa mbichi.
-Kanisa halikumkubali na kipaji chake
-Maisha yake yote hakujua wala kuhisi kama angekuwa maarufu.
-Ni yatima.
-Wamezaliwa watatu, wa kiume wawili na wa kike mmoja.
-Alisaidiwa na rafiki zake kuweza kuingia studio.
-Aliokoka mwaka 2001.
-Aliishi akilea familia ya watu saba.
-Wasambazaji ndio wapanga bei ya kazi.

Albamu
Albamu yake ya kwanza ina nyimbo nane ambazo ni ‘Ni Kwa Neema na Rehema’, ‘Tarajia Mujiza’, ‘Asante Yesu’, ‘Usiwe Mbali Nami’, ‘Bwana Yesu’, ‘Atanifuta Machozi’, ‘Milele Usifiwe’ na ‘Mungu Wetu Anaweza’.
Akizungumzia ujio wa albamu yake mpya, Edson anasema itakuwa na wimbo ambao utatoka Desemba
mwaka huu.
Anasema albamu hiyo itaitwa kwa jina la ‘Amenihurumia asilimia mia’, ikiwa pia na nyimbo kama ‘Nikiwa na umri wa miezi Nane’, ‘Kweli ni Mimi’, ‘Mkono Wako’, ‘Uwe Nami’, ‘Nitamwimbia Bwana’, ‘Wewe ni Mshindi’, ‘Mtetezi Wetu yu Hai’, ‘Tumia Vizuri Nafasi’ na ‘Kyala Nnunu’.
Anasema kuwa albamu hiyo ameirekodi Cke Studio ikiwa na mahadhi mbalimbali kama rhumba, kwaito, zouk na sebene na itasambazwa na Umoja Vision.
Kuhusu wapenzi na mashabiki wa Morogoro kumhitaji katika Tamasha la Krismasi, litakalofanyika Uwanja  wa Jamhuri, Desemba 26, anasema bado hajapata mwaliko wa kushiriki.
Lakini anasema kwa vile ni tamasha kubwa la kumwimbia Mungu, angefurahi kama angepata nafasi hiyo ya kujumuika na wengine siku hiyo.
“Nawashukuru wapendwa, wapenzi na mashabiki wa nyimbo za Injili wa  Morogoro kwa kunikubali, lakini
sijapata mwaliko,” anasema Edson.
Hata hivyo, anadokeza kuwa aliwahi kupigiwa siku na waratibu wa tamasha hilo, Kampuni ya Msama Promotions, lakini bado anasubiri mwendelezo.
Tamasha hilo litakaloanzia Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Desemba 25, mbali ya Morogoro litafanyika pia Kilimanjaro, Dodoma na Arusha.

No comments:

Post a Comment